Gazeti la Mwananchi Kurudi Tena kwa Kishindo

0
110
Gazeti la Mwananchi Kurudi Tena

Huku wadau wa tasnia ya habari wakizidi kuipigia kelele serikali kuhusu sheria kandamizi zinazominya uhuru wa wanahabari, gazeti la Mwananchi lililofungiwa na serikali  wiki mbili zilizopita linajiandaa kurudi kikamilifu barabarani mapema kesho.

Katika mkutano na waandishi wa habari leo mchana, mkurugenzi mtendaji wa Mwananchi Communications Limited (MCL), Tido Mhando, ametangaza Mwananchi linarudi kwa kishido, likielekeza nguvu zake katika kuelimisha na kuhabarisha umma.

“Tunapenda kuwakumbusha wasomaji [kwamba] wataendelea kupata gazeti lenye habari za uhakika zilizojikita kwenye umahiri, uhuru na weledi wa uandishi na uhariri,” inasema taarifa iliyotolewa kutangaza kurudi rasmi kwa Mwananchi.

Vilevile, Bwana Mhando amethibitisha kuendelea kwa promosheni ya Chomoka na Mwananchi na kwamba kuanzia kesho  wasomaji wajiandae kushiriki na kujishindia zawadi kem kem kama ilivyokuwa kabla ya kifungo.

“Zawadi za milioni moja kila siku, na zawadi za magari mapya, zitaendelea kushindaniwa [ili] kutimiza ahadi yetu ya kutoa zawadi [za] jumla ya Sh 250 milioni,” inaongeza taarifa hiyo ya MCL.

Kwa takribani siku 14, wadau mbalimbali wamekuwa wakipinga vikali kufungiwa kwa Mwananchi na Mtanzania, ambalo serikali imelitwanga adhabu ya kutochapishwa kwa siku 90 ikilihusisha na utoaji wa habari iliyoitwa ya uchochezi.

Vilevile, mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu unaowakilisha  mashirika zaidi ya 50 yasiyo ya kiserikali, yaliungana kulaani kitendo cha Serikali kuyafungia magazeti ya Mwananchi na Mtanzania.

Kilio cha taasisi hizo kilirudiwa na Umoja wa Ulaya (EU), ambao ulihoji kupotea kwa uhuru wa vyombo vya habari Tanzania, huku ukiitaka serikali iboreshe sheria ya habari ya mwaka 1976 ili iweze kuakisi matakwa ya dunia ya sasa.

Chanzo: Tovuti ya Mwananchi

Toa maoni yako juu ya Gazeti la Mwananchi Kurudi Tena kwa Kishindo kwa kutumia nafasi hapo chini ilipoandikwa ACHA MAONI

Leave a Reply