SABABU 20 ZA CCM KUSHINDWA UCHAGUZI MKUU 2015 HIZI HAPA

0
1680

Na Thobias Odhiambo

SABABU 20 ZA CCM KUSHINDWA UCHAGUZI MKUU 2015 HIZI HAPA

Mimi ni mwanaCCM kindakindaki na ni mtu nisiyependa kupindisha mambo….nyeupe naiita nyeupe na nyeusi naiita nyeusi….sina unafiki hata tone! Nimetafakari kwa kina sana na kubaini kwamba kuna sababu takribani 20 zitakazopelekea chama changu cha CCM kushindwa uchaguzi mkuu wa mwaka huu wa 2015. Katika makala haya (Part One) nitaelezea sababu kumi na katika makala yatakayofuata hivi punde nitaelezea sababu zingine 10 zinazobaki. Kusema kweli chama changu kina hali mbaya sana mwaka huu ijapokuwa wanaCCM wenzangu hawataki kusema ukweli. Naona dhamira inanisuta kwa kuendelea kukalia ukweli huu pasipo kuuweka wazi ili wanaCCM wenye mapenzi mema na chama chetu waweze kutafakari kwa kina na hatimaye kutafutia ufumbuzi ili walau tuweze kupata 40% ya kura zitakazopigwa mwaka huu. Nionavyo mimi ni vigumu sana kwa chama changu kupata walau 30% ya kura katika uchaguzi huu. Naona kadri siku zinavyokwenda kitanzi kinazidi kukaza shingoni mwa chama changu. Kila siku huwa najiuliza, “ Hivi CCM tutaficha wapi aibu zetu mwaka huu?”. Natamani baada ya uchaguzi niikimbie nchi ili kuficha aibu hii.

Zifuatazo ni sababu 10 kati ta 20 zitakazopelekea chama changu cha mapinduzi (CCM) kushindwa uchaguzi mkuu Oktoba, 25:

1. TUHUMA ZA UFISADI
Wapinzani wetu wa kisiasa (UKAWA) wamefanikiwa kuitumia kete hii vizuri kwa kuwafahamisha wananchi kinagaubaga kuhusu tuhuma za ufisadi zinazokiandama chama chetu, hasa pale walipofanikiwa kuuaminisha umma wa watanzania kwamba ufisadi wa CCM ni wa kimfumo, sio wa mtu mmoja mmoja. Hoja hii ni ya kweli kwa 80%, kwa kuwa chama ni watu na haiwezekani wanachama wote wakawa wasafi. Nakiri kwamba hii hoja ni nzito na ni ya kweli. Naomba wanaCCM wenzangu tukubaliane na hili na hatimaye tutafute namna ya kukisafisha chama mbele za wananchi ili tuweze kuchagulika tena. Tangu zamani chama chetu kimekuwa kikitumbukia kwenye tuhuma hizi mara kwa mara lakini badala ya kulishughulikia tatizo hili tumeacha lizidi kushamiri na kukomaa. Hapa ndipo watanzania walipoanza kupoteza imani na chama chetu.

2. MAFISADI KUSHINDA KURA ZA MAONI
Kuna baadhi ya makada kwenye chama chetu wanaojulikana kwa sifa (mbaya) ya ufisadi lakini wameshinda kura za maoni kwa kutumia hila na chama chetu kitawapitisha kugombea ubunge. Siana haja ya kuwataja makada hao kwa kuwa wanajulikana bayana kwa kila mtanzania. Wamo waliohusika na ufisadi wa rada, EPA na hata ESCROW lakini bado chama chetu kinazidi kuwakumbatia badala ya kuwafukuza na kuwavua uanachama. Tabia hii ya chama chetu kuwaabudu na kuwasifu mafisadi imepelekea wananchi kukata tamaa. Hata viongozi wanaposimama majukuwaani na kukemea mafisadi wakati wamejaa tele ndani ya chama wananchi hawatuelewi hata kidogo. Hili ni kosa kubwa sana litakalochangia kwa kiasi kikubwa kutuangusha kwenye uchaguzi wa mwaka huu. Ukumbatiaji wa mafisadi ndani ya chama ni kansa itakayokigharimu chama chetu. Hii tabia ya kuzoa kila aina ya waovu na kuwaingiza ndani ya chama inawachefua sana wananchi ambao ndio wapiga kura wetu.

3. RUSHWA KWENYE CHAGUZI ZA NDANI
Tangu uteuzi wa mgombea wa urais kwa tiketi ya chama chetu, kashfa ya rushwa na ununuzi wa wapigakura imekuwa ikishamiri, kukua na kuota mizizi. Kumbukuka yule mhidi aliyekamatwa na viroba vya noti akitaka kuwahonga wajumbe wa mkutano mkuu ili kuwashawishi wajumbe wampigie kura mtu anayetakiwa na kikundi kidogo cha watu. Sitaki kuingia kwa undani zaidi kwenye sula hili hasa ukizingatia namna lilivyomalizwa kwa aibu huku mwanaCCM aliyehusika kugawa zile noti akishinda kura za maoni ya kugombea udiwani katika jimbo jipya la Mbagala. Ni aibu sana kwa chama chetu.

Chaguzi zetu za ndani mwaka huu zimegubikwa mno na rushwa huku baadhi ya makada wakiwanunua wapiga kura na kucheza rafu za hapa na pale ilmradi tu waingie madarakani. Tumeshuhudia wagombea wakitengeneza kadi feki na kuwagawia mamluki waliowapigia kura na kisha kushinda kura za maoni. Na kwa kuwa katibu mkuu wetu, Bwana Kinana, amesema kwamba hawatarudia makosa ya mwaka 2010, ni dhahiri kwamba wagombea wote waliopita kwa rushwa watateuliwa kupeperusha bendera ya chama chetu dhidi ya UKAWA. Hili ni kosa kubwa sana kisiasa. Haiwezekani wananchi wameshuhudia namna kura zilivyokuwa zikinunuliwa kama njugu halafu uwapelekee wagombea hao waovu kwamba wawapigie kura. Thubutu! Wananchi wa sasa sio kama wale wa enzi za Mwalimu Nyerere. Watatuangusha mchana kweupe! Kitendo cha ufisadi kushamiri chamani hadi kulazimisha kununua uongozi ni jambo la hatari sana litakalochangia kuanguka na hatimaye kufa kwa chama chetu. Nitoe rai kwa wanaCCM wenzangu watakaoshiriki vikao vya mchujo wawaondoe wagombea wote walioshinda kwa hila ama sivyo chama chetu kitaangamia.

4. UTEUZI WA MGOMBEA MWENZA MWANAMKE
Zaidi ya 51% ya wapiga kura wote hapa nchini ni wanawake. Kwa maana hiyo, CCM tulitumia kete ya kuteua mgombea mwenza mwanamke kwa ajili ya kuvutia kura za wanawake. Hili ni kosa kubwa sana. Kwa kawaida wanawake hawapendani wao kwa wao. Ni rahisi mpigakura mwanamke kumpigia kura mgombea wa kiume kuliko mwanamke mwenzake. Na kitendo hiki cha kuteua mgombea mwanamke kwa malengo “chanya” sasa kitageuka kuwa shubiri kwa chama chetu. Na kitapelekea wanawake kuwapigia kura wagombea wa UKAWA badala ya CCM. Kwanni nasema hivyo? Ni jambo lililo wazi kwamba mwanamke huwa hapendi kuona mwanamke mwenzake anakuwa juu au anapiga hatua zaidi yake. Hii ni hulka ya kijenetiki ambayo haiwezi kubadilishwa na binadamu yeyote. Kama busara ingetumika tangu zamani tungeweza kuepuka kikwazo hiki mapema lakini kwa kuwa tayari mgombea alishathibitishwa, hakuna jinsi zaidi ya kujiandaa kisaikolojia kwa lolote litakalotokea.

5. “MAISHA BORA KWA KILA MTANZANIA”
Wakati Rais wetu Kikwete anaingia madarakani aliwaaminisha wananchi kwamba watapata “MAISHA BORA KWA KILA MTANZANIA”. Lakini mpaka rais wetu anaondoka madarakani, hakuna jipya lililofanyika. Maisha yamekuwa magumu mara 20 zaidi ya ilivyokuwa kabla chama chetu cha CCM hakijaingia madarakani mwaka 2005. Ugumu wa maisha unabainishwa na kupanda kwa gharama za bidhaa sokoni. Nakumbuka wakati rais anaingia madarakani mwaka 2005 kilo moja ya sukari ilikuwa inauzwa Tsh 300. Mpaka anaondoka madarakani hivi sasa bei ya sukari ni Tsh 2,000. Bei imepanda kwa 500%. Hii maana yake ni kwamba ugumu wa maisha pia umeongezeka kwa kiwango hicho. Katika hali kama hii ni mwananchi gani atakayekubali kudanganywa tena safari hii? wanaCCM wenzangu naomba tujipange sawasawa tutafute majibu tutakayoenda kuwaambia wanachi wakati tunaenda kusaka kura mwaka huu maana nina uhakika kwamba tutakumbana na maswali mengi sana huko mtaani hasa kuhusu kupanda kwa gharama za maisha, jambo ambalo limekwenda kinyume na kaulimbiu yetu ya “MAISHA BORA KWA KILA MTANZANIA”. Tujitafakari kwanza kabla ya kwenda kusimama mbele ya wanachi tukiwaomba kura.

6. KUHAMA KWA LOWASSA
WanaCCM wengi tunabeza kuondoka kwa Lowassa hadi kufikia kumuita eti ni kapi! Tunajidanganya sana ndugu zangu. Mh Lowassa bado ana nguvu nyingi na kadri tunavyozidi kumchafua ndipo nyota yake inazidi kung’ara. Tazama jinsi wanaCCM wenzetu wanavyohama chama na kujiunga UKAWA. Hamjiulizi kwanini? Ni mwendawazimu pekee anayeweza kubeza nguvu za kisiasa za Mh Lowassa. Kosa tulilolifanya kukata jina lake tutalijutia milele na litatugharimu pakubwa. Wakati Lowassa anatafuta wadhamini kupitia chama chetu alipata wadhamini zaidi ya milioni moja na kuna mamilioni ya wengine ambao wanamuunga mkono lakini hawakupata nafasi ya kumdhamnini. Ni dhahiri kwamba hata baada ya kuhama lazima atahama na mamilioni kadhaa ya wanaCCM mioyoni mwao ijapokuwa bado wanajifanya wapo ndani ya CCM. Hawa ndio watakaotuangamiza siku ya uchaguzi. Tutarajie na tujiandae kulipukiwa na bomu hili. Nadhani nimeeleweka vizuri.

7. UVAMIZI
Lengo na madhumuni ya kuanzishwa kwa TANU na hatimaye CCM lilikuwa kuwakomboa wanyonge. Hivi sasa tumeshuhudia chama chetu kikivamiwa na mafisadi na watu wachache walio tayari kuingia madarakani kwa nguvu za fedha. Kwa sasa ni vigumu mkulima wa kawaida asiyekuwa na uwezo wa kifedha kupata uongozi ndani ya chama chetu. Hii maana yake nini? Inaashiria kwamba sasa chama hiki ni cha watu wachache wenye fedha wanaoweza kuwanunua wapigakura na kushinda uchaguzi kiulani kwa manufaa yao binafsi—sio kwa manufaa ya kuwatumikia wananchi. Wananchi wa kawaida, ambao ndio wengi, wamegundua hilo na kujitenga mbali kabisa na chama. Wanakiona chama hakina manufaa kwao tena zaidi ya wachumiatumbo wachache ambao wamekigeuza chama chetu kuwa kampuni yao binafsi ya kuchumia fedha na maslahi binafsi. Jambo hili limejenga chuki kwa wananchi wa kawaida hivyo kupelekea kukichukia chama chetu huku mwakisubiri kuonyesha hasira zao hizo kupitia sanduku la kura. Nimshukuru katibu mkuu wetu kwa kujitahidi kukifufua chama lakini jitihada zake zimekosa sapoti.

8. UONGO, UNAFIKI NA UZANDIKI
WanaCCM wenzangu ni hodari sana kwa kutunga uongo na kuulazimisha kuwa ukweli. Hili ni kosa kubwa sana. Wananchi wa sasa wameamka. Huwezi kuendelea kuwadanganya kama watoto wadogo ukitegemea kwamba watakuwelewa. Mfano halisi ni pale tunapojaribu kuwaaminisha kuwa chama chetu bado kina uwezo wa kuendelea kuwatumikia wananchi wakati tukitambua fika kwamba chama kimechoka na kimeshindwa kuleta mwanga wa matumaini kwa watanzania. Tuache unafiki ndugu zangu. Hata punda hana akili lakini ukimbebesha mizigo mizito sana, ipo siku atakugezia kibao akukupiga mateke ya tumbo na kukupasua bandama. Tunapaswa kutambua kwamba wananchi wamekichoka chama chet. Hawana hamu nacho tena. Tujipange na kujitafakari namna ya kurejesha imani ya watanzania kwa chama chetu.

9. VIJIWE VYA KAHAWA
Ukipita katika vijiwe vingi vya kahawa na visivyo vya kahawa vinavojadili masuala ya siasa utagundua kwamba Lowassa anaungwa mkono na zaidi ya 98% ya wananchi. Katika vijiwe vyote nilivyopita utamkuta mtu mmoja anayemuunga mkono mgombea wa CCM huku 99 waliobaki wanamuunga mkono Lowassa. Katika akili za kawaida hata bila kuingia mtaani kufanya utafiti wa kina utagundua wananchi wengi wana imani na Lowassa ambaye ni mgombea wa UKAWA dhidi ya Magufuli, mgombea wa chama chetu cha CCM. Sihitaji kwenda mbali zaidi kwenye hoja hii kwa kuwa ukweli unajidhihirisha wazi.

10. UTAFITI WA REDET
Katika utafiti uliofanywa na REDET , TWAWEZA na watafiti wengine, nyota ya Lowassa bado inazidi kung’ara. Utafiti huo ulionyesha kuwa Lowassa anaongoza, akifuatiwa na Dr Slaa. Kwa kuwa sasa Lowassa yupo kambi moja na Dr Slaa. Ni wazi nguvu zao zimeunganishwa pamoja ndani ya UKAWA na hivyo kuzidi kuwang’arisha zaidi. Badala ya kutafuta mbinu ya kumg’arisha mgombea wa chama chetu, Dr Magufuli, tumekazana na Lowassa kila kukicha. WanaCCM wenzangu tujitazame upya. Siasa za majitaka zimeishapitwa na wakati. Badala ya kuwarubuni polisi kuvamia maandamano ya UKAWA, tujumuike pamoja kujenga chama chetu ili tuone kama tutashinda uchaguzi wa mwaka 2020 kwani uchaguzi wa mwaka huu tayari tumeishaangukia pua.

ANGALIZO
Mimi ni miongoni mwa wanaCCM wachache wanaoweza kuthubutu kusema ukweli bila kupepesa macho wala kutikisa masikio. Mwalimu Nyerere aliwahi kutuasa kwamba mtu anayeficha ugonjwa huumbuliwa na kilio. Ndugu zangu naomba tujitafakari na tujisahihishe. Tusiangalie pale tulipoangukia pale tuangalie tulipojikwalia. Msema ukweli ni mpenzi wa Mungu. Sasa hivi chama chetu kina hali mbaya sana. Ni vema tukiri ukweli huo na tuanze kujkijenga chama kuanzia sasa tukijiandaa kushika dola tena mwaka 2020, mwaka huu hatuna chetu. Afadhali nionekane mbaya kwa kusema ukweli kuliko kuwa mnafiki kwa kukumbatia uongo, unafiki, uzabizabina na uzandiki. Nimetumbua jipu pwaaaaaaa!

ACHA MAONI

Please enter your comment!
Please enter your name here