Ukweli kuhusu Dr Lous Shika wa Mnada wa Nyumba za Lugumi huu hapa

0
0
Image may contain: 1 person, standing

Kutoka JamiiForums.!
_____________________
Nimeguswa sana na tukio la kushikiliwa na vyombo vya dola mtu anayetajwa kama Dr Louis Shika (pichani) ukiacha tukio lilivyo, mtu huyo ninamfananisha sana na "SHIKA LUNYALULA KIDOLA" mzaliwa wa kitongoji cha CHAMUGASA kijiji cha KALEMELA wilaya ya BUSEGA, Simiyu.
Nimeona hata passport ya Dr.Louis Shika kwenye jina la ubin (surname) imeandikwa Kidola. Kwahiyo huenda ni yeye.
Shika ninayemfahamu, ni ndugu yake JEREMIAH SHIKA KIDOLA. Hawa wawili waliakuwa miongoni mwa wanafunzi wenye akili sana na waliofaulu vizuri masomo yao ya sekondari kwa alama za juu na kupata ufadhili wa kwenda kusoma udaktari nchini Urusi.
Walikuwa wanafunzi wa vyuo vikuu huko USSR (Urusi ya zamani) mwishoni mwa miaka ya 1980 hadi mwanzoni mwa miaka ya 1990, ambapo walirejea nchini na kuanza kutibu katika hospitali ya taifa ya Muhimbili.
Nakumbuka wote wawili Dr.Louis na Dr.Jeremiah Shika (ambaye ni marehemu kwa sasa), walisoma udaktari bingwa huko Urusi. Dr.Jeremiah ndiye aliyetangulia kuwa daktari bingwa na aliporudi alifanya kazi kidogo Muhimbili na baadae aliajiriwa kuwa miongoni mwa madaktari bingwa (Specialist) wa mwanzomwanzo pale Bugando Hosptital Mwanza.
Dr.Louis yeye alihudumu kwa muda kama daktari wa kawaida (MD) kabla baadae hajaenda kujiendeleza zaidi nchini Urusi na kusomea udaktari bingwa. Sina hakika sana alispecialize kwenye nini lakini kama sikosei ni magonjwa ya akili (psychiatrist).
Binafsi nina zaidi ya miaka 30 bila kuonana na Dr.Shika, ingawa ilijulika mapema kuwa alioa mke wa Kirusi alipoenda kusoma masomo yake ya juu, na baadaye kuzama kwenye ulevi wa pombe za kupindukia huko Urusi.
Mwaka juzi nilikutana na mgodo wao Daudi Shika aishiye kijiji cha Mwamanga – Magu, akanijulisha kuwa, DR.SHIKA alisharudi Tanzania lakini alidai akili zake hazina utimamu tena.
Daudi akaniambia Dr.Shika alirudi nchini mwanzoni mwa miaka ya 2000 lakini hawajui kama alihitimu masomo yake ya udaktari bingwa au alikatisha. Japo zipo taarifa kuwa hakuhitimu kutokana na ulevi wa kupindukia na akili yake kuonekana haiko sawa, na alirudishwa kwa amri ya serikali.
Kwahiyo ana zaidi ya miaka 15 tangu arudi nchini lakini kila siku anadai kusubiri mizigo yake kutoka Urusi ifike bandarini. Alinieleza kuwa kaka yao (Dr.Louis) alikuwa hajui kwa nini mizigo yake imechelewa kufika hali ambayo ilidaiwa kumsababishia msononeko mkubwa sana.
Daudi aliniambia kuwa ilikuwa zaidi ya miaka 12 tangu Baba yao mzee Lunyalula Kidola afariki dunia (mwaka 2005), lakini kaka yao Dr.Louis hakuwahi kufika msibani licha ya kuwepo Dar es Salaamu. Hata mawasiliano na ndugu zake kijijini ni kwa nadra sana na mara nyingi ni hadi wao wamtafute. Wakiongea nae kwenye simu huwaambia wamsalimie baba yao licha ya kuwa alifariki miaka mingi iliyopita.
Nimesikia Kamanda wa Polisi Dar, SACP Mambosasa akisema kuwa polisi wamefuatilia na kugundua kuwa Dr.Shika hana makazi ya kudumu jijini Dar es Salaam. Anaishi kwenye chumba kimoja cha kupanga na anadaiwa malimbikizo ya kodi.
Kifupi, nimeguswa sana na jina la SHIKA pia sura yake kama mtu ninayemfahamu vizuri tangu tukiwa majirani kijijini wakati huo Shika na Jeremiah wakisoma darasa moja kwenye Shule ya msingi Chamugasa pamoja na dada yangu mkubwa Magdalena. Hivyo, sura hii ndiyo sura pia ya mdogo wake aliyeko kijijini Chamugasa aitwaye Pius na mdogo wao mwingine Daudi.
Ikiwa huyu ndiye Dr.Shika ninayemfahamu, daktari bingwa wa magonjwa ya akili basi nimeumizwa mno na mfumo wa maisha yake. Licha ya kwamba tunatoka kijiji kimoja lakini kama mtanzania wa kawaida sikutegemea daktari bingwa awe katika maisha haya.
Kuna watu wanaweza kumbeza Dr.Shika lakini hatujui nini kilimpata. Hatujui huko Urusi alifanyiwa nini. Hatujui huyo mwanamke aliyemuoa huko ilikuaje wakaachana. Hatujui kama walifanikiwa kupata watoto. Hatujui kwanini serikali ilishindwa kumsaidia Dr.Shika wakati ilitumia kodi za watanzania kumsomesha nje ya nchi.
Bila shaka Dr.Shika alipaswa kuwa katika nafasi ya kuisaidia jamii yake kupitia elimu yake. Ilitegemewa sasa hivi awe daktari mwandamizi mshauri, ambaye madaktari junior wanaenda kupata maelekezo kwake. Au alipaswa kuwa mhadhiri chuo kikuu cha Sayansi ya tiba kama MUHAS, CUHAS au KCMC akihamisha maarifa yake ya udaktari kwa wanafunzi wa udaktari.
Lakini yupo mjini tu anahangaika. Anaishi chumba kimoja peke yake. Hana mke, hana mtoto, hana nyumba, hana gari, hana mifugo. Yuko peke yake.
Hatimaye ameingia kwenye biashara ya utapeli. Kutoka udaktari bingwa hadi utapeli. Na afya yake inavyoonekana ni mlevi wa kupindukia hadi midomo imebabuka. Huenda anakunywa pombe kali za kienyeji kama chang'aa na mataputapu mengine. Pia inawezekana hana muda wa kula. Mtu anayeishi peke yake atapika saa ngapi? Nani atamkumbusha kula? Lazima afya yake itadorora.
Bila shaka hakupenda kuwa katika hali hiyo. Huenda yupo kwenye msongo mkubwa wa mawazo. Kwa kifupi Dr.Shika si timamu tena. Anahitaji usaidizi wa hali na mali.
Kumdhihaki na kumuacha apotee haitasaidia kitu. Zaidi sana taifa ndio litapata hasara kwa kutumia rasilimali zake kumsomesha mtu aliyegeuka mzigo kwa taifa. Mimi naamini Mwalimu Nyerere alipowasomesha Shika na kaka yake alikuwa ana matumaini makubwa nao, kwamba watasaidia taifa. Hebu fikiria Shika angekuwa timamu angesaidia watu wangapi? Leo kuna watu wanakufa kwa kukosa madaktari, lakini kuna madaktari kama Dr.Shika wapo tu mtaani hawajielewi, wameangukia kwenye ulevi wa kupindukia na utapeli.
Serikali iangalie namna ya kuwasaidia watu wa aina hii kwa maslahi ya taifa. Naamini hata madaktari waliosoma na Shika Urusi, au waliofanya nae kazi Muhimbili wana nafasi ya kumsaidia kama wataamua kufanya hivyo.

Toa maoni yako juu ya Ukweli kuhusu Dr Lous Shika wa Mnada wa Nyumba za Lugumi huu hapa kwa kutumia nafasi hapo chini ilipoandikwa ACHA MAONI

Leave a Reply